Mto Malagarasi ndoto imetimia: Rais Kikwete


Rais Kikwete, akikata utepe kuashiria uzinduzi wa daraja la Mto Malagarasi, wilayani Uvinza.

Rais Kikwete, akikata utepe kuashiria uzinduzi wa daraja la Mto Malagarasi, wilayani Uvinza.

 

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzani, Dkt. Jakaya Kikwete, amezindua Daraja la Mto Malagarasi na kuashiria kukamilika na serikali kuupokea rasmi mradi wa daraja hilo lenye urefu wa mita 275 kutoka kwa mkandarasi Kampuni ya Hanil Engineering kutoka nchini China, iliyolijenga.

Akiongea wakati wa kuzindua daraja hilo, Rais Kikwete, alisema kuwa  daraja hilo linaufungua mkoa wa Kigoma na kuunganisha na miko mingine ya Tanzania pamoja na kuwaondolea adha wananchi wa mikoa ya ukanda wa Magharibi kwa mawasiliano.

Alisema kuwa daraja hilo ni miongoni mwa madaraja matano ambayo serikali ya awamu ya kwanza ilipanga kuyajenga katika mpango wa kwanza wa maenedeleo chini ya Hayati Mwalimu Julius Nyerere na kwamba kukamilika kwake serikali ya awamu ya nne inajivunia kutekeleza ndoto ya muasisi wa Taifa.

“Baba wa Taifa alidhamiria na alitamani lijengwe katika kipindi chake cha uongozi, hakufanikiwa, lakini kizazi cha viongozi tuliofuatia tumelijenga hili daraja, kwa jambo linguine la faraja kwangu ni kwamba tumeitekeleza ndoto ya muasisi wa taifa letu na mlezi wa sisi wengine wote,”alisema Rais Kikwete.

Aidha Rais Kikwete alisema kuwa baada ya kukamilika kwa daraja hilo na barabara unganishi ya kiwango cha lami yenye urefu wa kilomita 48, serikali sasa inashughulika na barabara ya kutoka Kidahwe kwenda Nyakanazi yenye urefu wa kilomita 300 ambapo benki ya Maendeleo ya Afrika imekubali kusaidia.

 

E80A9576

 

Awali Mkurugenzi Mtendaji wa Wakala wa Barabara nchini TANROAD, Eng. Patrick Mfugale, alisema mradi wa ujenzi wa daraja hilo lililopewa jina la Daraja la Kikwete, umegharamiwa kwa pamoja na serikali ya Korea Kusini kupitia mfuko wake wa maendeleo na serikali ya Tanzania.

Alisema mfuko wa maendeleo wa serikali ya Korea Kusini umechangia asilimia 78.3% ya gharama nzima na serikali ya Tanzania imechangia asilimia 21.7 ikiwa ni pamoja na fidia kwa watu waliothirika na mradi huo na kwamba gharama nzima za ujenzi wa daraja hilo ni bilioni 90.9 na mkandarasi ameshalipwa bilioni 78.234.

Aidha Eng. Mfugale, alisema kuwa mkandarasi amekamilisha kazi ya ujenzi tangu Novemba 18, 2013, ndani ya mkataba na kipindi cha uangalizi cha miaka mitatu kinaishia Novemba 18, 2016.

Akimwakilisha Waziri wa Ujenzi John Magufuli, kwenye uzinduzi huo, Waziri wa Ardhi , Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi, alisema katika awamu ya nne chini ya Rais Kikwete, serikali imetekeleza na inaendelea kutelekeza miradi ya barabara yenye urefu wa kilomita 17, 762 na kati ya hizo barabara zenye urefu wa kilomita 5,568 zimekamilika kujengwa kwa kiwango cha lami.

Aidha kilomita 3,873 zinaendelea kujengwa kwa kiwango cha lami na kilomita 4, 965 zimefanyiwa upembuzi  yakinifu na kilomita 3, 356 kufanyiwa usanifu wa kina na kwamba serikali ya Rais Kikwete imetumia kiasi cha shilingi Trillioni 9 kwa ajili ya ujenzi wa miradi ya barabara toka mwaka 2005.

Nae Balozi wa Korea Kusini  hapa nchini, IL Chung, akitoa shukrani za pekee kwa wafanyakazi wote walioshiriki katika ujenzi wa daraja hilo na kuwezesha wananchi kupita misimu yote na kuongezeka kwa biashara kwa kiasi kikubwa na kwamba kwa sasa Kigoma imekuwa kitovu cha Afrika Mashariki.

Aliongeza kuwa Tanzania itakuwa nchi yenye maendeleo makubwa kama itatumia rasilimali zake ikiwemo uwezo wa watu wake na Teknolojia.

By KigomaLive Posted in Habari

Toa Maoni Yako Kuhusu Habari Hii