Wasimamishwa kazi kwa kuudanganya Mwenge


WATUMISHI 6 wa serikali wakiwemo makaimu wakurugenzi wa Manispaa ya Kigoma Ujiji na Maafisa wa Maendeleo ya Jamii wa Halmashauri ya Wilaya ya Kigoma, wamesimamishwa kazi kwa tuhuma za kujihusisha na udanganyifu katika miradi iliyokuwa ikizinduliwa na Mwenge wa Uhuru.

Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Brigedia Jenerali Mstaafu, Emmanuel Maganga, alisema wakati wa kukimbiza Mwenge katika mkoa, kumejitokeza mambo yasiyofaa ya kuwatumia vijana na kikundi hewa cha SACCOS kuwakilisha kuonyesha kuwa upo mradi wa nyuki na kuchakata asali ambao umefadhiliwa na halmashauri ya wilaya ya Kigoma.

Alisema baada ya uchunguzi wa awali kufanyika ikiwa ni pamoja na kuwahoji vijana hao hawakuwa na majibu yoyote hivyo ilibainika kuwa ule mradi ni mradi wa familia na wale vijana walikusanywa tu waje kuonyesha kwamba wao ni sehemu ya huo mradi.

Udanganyifu huo umebainika wakati Mwenge ulipokimbizwa katika kijiji cha Mahembe,wilayani Kigoma, ambapo maafisa wa idara ya maendeleo ya jamii wa halmashauri hiyo Prosper James Ntana na Alex Dismasi Ntiboneka, ndio wamehusishwa na udanganyifu huo hivyo wamesimamishwa kazi kupisha uchunguzi.

Alisema katika tukio lingine la udanganyifu kiliandaliwa kikundi hewa cha SACCOS, kilichoitwa SACCOS ya Vijana Manispaa ya Kigoma Ujiji, ambacho pia kilipewa hundi hewa ya zaidi ya shilingi milioni mbili ikiwa haina saini, wakati jina la kikundi halali chenye usajili na kinachotambulika ni Kigoma Ujiji Vijana SACCOS.

Waliosimamishwa kazi katika tukio hilo la pili ni Dk.Revocatus Masanja na Sultani Ndoliwa makaimu wakurugenzi wa Manispaa ya Kigoma Ujiji, na Rabani Ghwahuzu na Ajira Jabir ambao ni maafisa maendeleo ya jamii Manispaa ya Kigoma Ujiji.

Kufuatia vitendo hivyo mkuu wa mkoa Brigedia Maganga, ameziagiza mamlaka za nidhamu za watumishi hao ziwachukulie hatua za kinidhamu ili kupeleka salaam kuwa suala la mwenge linahitaji kuchukuliwa kwa uzito mkubwa.

“Tuliunda kamati ya mkoa pamoja na kamati za wilaya za mwenge; msisitizo ulikuwa ufanyike ukaguzi madhubuti kuhakikisha kwamba wakati tunakimbiza huu mwenge kusitokee vitendo visivyofaa, lakini jana (juzi) kumetokea mambo yasiyofaa,”alisema Brigedia Maganga.

“Suala la Mwenge ni suala zito, ni suala la kitaifa na kila mtu Tanzania nzima toka huko Morogoro ulipowashwa wameusimamia kwa makini na kuhakikisha kwamba vitendo vyote vinavyotakiwa kufanyika, vinafanyika na sio kuingiza udanganyifu.”

Aidha Brigedia Maganga, amemwagiza Katibu Tawala wa Mkoa kuwachukulia hatua zilizo ndani ya mamlaka yake wajumbe wa kamati ya Mwenge ya Mkoa ambao gharama kubwa zilitumika kuwawezesha kutembelea miradi yote ya mkoa ambayo Mwenge ungepita na katika kikao cha majumuisho walimhakikishia mkuu wa mkoa kuwa miradi yote iko vizuri.

 

 

 

By KigomaLive Posted in Habari

Toa Maoni Yako Kuhusu Habari Hii