Wahitimu Darasa la 7 wajinasibu kufaulu masomo ya Sayansi


WAKATI mitihani ya kumaliza elimu ya msingi ikimalizika leo kote nchini, baadhi ya Wanafunzi wamezungumzia namna mitihani ilivyokuwa huku wengi wakionekana kuhamasika zaidi na kujiamini kufaulu masomo ya Sayansi na Hisabati.

Wakiongea na Mtandao huu, baadhi ya wanafunzi wa Shule ya Msingi Burega iliyopo Manispaa ya Kigoma Ujiji, wakiwemo Alex Abel, Elius Paul na Nairat Amri, wamesema mitihani ilikuwa mizuri na wana uhakika wa kufaulu.

Wamesema hakuna kipya kichokuja kwenye mitihani ambacho ni tofauti na kile walichofundishwa na walimu wao tangu mwezi Januari hadi Septemba.

Kuhusu masomo ya Sayansi na Hisabati wengi wa wahitimu hao wameonyesha kujiamini kufanya vizuri huku wengi wao wakieleza ndoto zao za kuwa madaktari.

Kwa upande wake Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Burega Vivian Msindai, amesema ana imani kwamba watoto wake watafaulu kwa kuwa waliwandaa vizuri kwa kuwapa mazoezi ya kila mwezi na wameonekana kupenda na kumudu masomo ya Sayansi na masomo mengine.

Amesema kuwa jumla ya wanafunzi 74 wakiwemo wasichana 33 wamefanya mitihani ya kuhitimu darasa la saba mwaka huu kati ya wanafunzi 90 walioanza darasa la kwanza, na kwamba wengine hawakumaliza kutokana na sababu mbali mbali ikiwemo utoro.

Nae Kaimu Afisa Elimu wa Mkoa wa Kigoma, Venance Babukege, amesema kuwa jumla ya wanafunzi elfu 28,197 wamefanya mitihani ya kuhitimu darasa la saba mwaka huu kwa mkoa wa Kigoma sawa na asilimia 70%.

Amesema kati yao wasichana ni elfu 14,460 na wavulana ni elfu 13,737, wakiwemo wanafunzi wasioona 4, wenye uoni hafifu 14.

Aidha amesema hadi kufikia siku ya mwisho ya mitihani hiyo hakuna kasoro yoyote iliyojitokeza wala tukio lolote la udanganyifu katika mitihani.

Jumla ya wanafunzi waliofanya mitihani ya kuhitimu darasa la saba mwaka jana kwa mkoa wa Kigoma ilikuwa elfu 31,191 ambapo ufalu ulikuwa asilimia 42% na kushindwa kufikia malengo ya Matokeo Makubwa Sasa ambayo ilikuwa asilimia 70%.

By KigomaLive Posted in Elimu

Toa Maoni Yako Kuhusu Habari Hii