RC aimwagia Sifa Timu ya Ngumi Kigoma


IMG_9432

Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Luteni Kanali Mstaafu Issa Salehe Machibya, amewapongeza Wachezaji na Viongozi wa Timu ya Ngumi ya Mkoa kwa Mafanikio waliyoyapata kwenye Mashindano ya Taifa ya ngumi za wazi yaliyomalizika hivi karibuni Jijijini Dar es Salaam.

Timu ya ngumi ya mkoa wa Kigoma ilikuwa ikishiriki mashindano hayo kwa mara ya kwanza lakini wapiganaji wake walifanikiwa kunyakua medali 9 zikiwemo 3 za dhahabu na kuwa washindi wa pili nyuma ya Ngome ya Dar es Salaam katika ushindi wa jumla.

Kufuatia mafanikio hayo Luteni Kanali Mstaafu Issa Machibya ametoa salaam za pongezi kwa wachezaji na viongozi wote waliokwenda kushiriki mashindano hayo kwa kuuletea sifa mkoa wa Kigoma kwenye medani ya mchezo wa ngumi.

“Nimefarijika sana na nichukue nafasi hii kuwapongeza sana kwa kutuletea ushindi mkoa wa Kigoma, tungeweza kuwa washindi wa kwanza lakini Ngome wao wana historia ya muda mrefu katika mchezo huu. Na wametushinda kidogo sana kwa hiyo kwenye mashindano yajayo tunaweza kuchukua,”alisema.

Aidha alisema tayari mkoa umeanza kuchukua hatua za kuwekeza katika mchezo wa ngumi ili uweze kupendwa kama michezo mingine kama vile mpira wa miguu na mipango inafanywa ili mkoa wa Kigoma uwe na ulingo kwa ajili ya mchezo wa ngumi.

Alisema amemuomba Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Dk.Fenella Mukangara kusaidia katika suala la ulingo na kama ombi hilo halitafanikiwa kwa wakati mkoa utatafuta fedha ikiwa ni pamoja na kuwashirikisha wadau katika kusaidia ulingo kupatikana.

Alisema kama kutakuwa na ulingo wa kudumu kwa ajili ya mchezo wa ngumi mkoa utakuwa na mashindano mengi ya ngumi yatakayoshirikisha wachezaji kutoka mikoa na nchi jirani na kwamba kwa kufanya hivyo vijana watahamasika kushiriki mchezo wa ngumi na pato la mkoa litaongezeka.

“Tunataka hii michezo hapa pia tuweze kuwavuta wenzetu wa Katavi, Tabora, Kagera, Geita na hata kutoka Burundi mchezo uchezewe hapa. Mchezo huu ukichezewa hapa (Kigoma), pato letu la mkoa litaongezeka na pia vijana wetu watahamasika na kushiriki mchezo huu kuanzia ngazi ya mkoa, Taifa na hatimaye mashindano ya kimataifa,”aliongeza.

Katika hatua nyingine Luteni Kanali Mstaafu Issa Machibya, alizitaka halmashauri zote za mkoa wa Kigoma waweke mipango ya kuwa na maeneo ya michezo na kumbi za michezo mbali mbali katika maeneo yao badala ya kuangalia tu maeneo ya stendi za magari.

Alisema sambamba na kuwa na ulingo ni lazima kuwa na maeneo ya kufanyia michezo mbali mbali, na kwamba safari hii waliomba ukumbi wa Magereza kwa ajili ya wachezaji wa ngumi, lakini wakurugenzi na wataalam wao wawe na upeo wa kutenga maeneo kwa ajili ya michezo ikiwa ni pamoja na kuwa kumbi za michezo.

“Sambamba na kuomba vifaa vya michezo lakini pia tumewaambia Manispaa pamoja na halmashauri zetu kutengeneza kumbi za michezo (Indoor & Outdoor),kuboresha na viwanja vya soka na michezo yote, hiyo ni katika kuweka mikakati ya kuhakikisha kwamba michezo hapa tunaifanya vizuri zaidi.

Katika mashindano ya Taifa ya ngumi ambayo yalikuwa maalum kwa ajili ya kumuenzi aliyekuwa Rais wa kwanza mzalendo nchini Afrika Kusini, Hayati Mzee Nelson Mandela, mkoa wa Kigoma ulipeleka mabondia 11 wa uzito mbali mbali huku 3 kati yao wakiwa mabondia wa kike.

Mabondia hao pamoja na uzito waliopigana kwenye mabano ni Fred Julius (Kg 81),Frank Msindo(Kg 69),Isihaka Moshi(Kg 60),Shabani Msumari (Kg 60), Ezra Paul (Kg 56) na Rashid Samvu (Kg 56) na Abbas Khamisi (Kg 49),upande wa Wavulana.

Mabondia Wasichana ni Latifa Khalid (Kg 52), Rudia Mashala (Kg 52) na Agnesi Moshi (Kg 75).

Waliopta medali za dhahabu ni Ezra Paul, Ageni Moshi na Latifa Khalid, wakati walionyakua medali za Fedha ni Abbas Khamisi, Frank Msindo, Fred Julius na Rudia Mashala.Medali za shaba zilinyakuliwa na Shabani Msumari na Isihaka Moshi.

Kwenye Mashindano hayo pia Timu ya Ngumi ya Mkoa wa Kigoma pia ilifanikiwa kupata kombe maalum kwa kuwa timu yenye nidhamu.

 

Toa Maoni Yako Kuhusu Habari Hii