Zaidi ya nusu ya wanafunzi hawajaripoti Shule Kigoma


Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Luteni Kanali Mstaafu Issa Salehe Machibya.

Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Luteni Kanali Mstaafu Issa Salehe Machibya.

 

Jumla ya wanafunzi 6,859 ambao ni sawa na asilimia 53% ya wanafunzi 12,878 ya waliochaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza mwaka 2014 kwenye Sekondari za kutwa katika Mkoa wa Kigoma, bado hawajaripoti shuleni tangu shule zilipofunguliwa Januari 6 mwaka huu.

Taarifa toka ofisi ya Elimu Mkoa wa Kigoma ambayo imetolewa kwa waandishi wa habari na Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Luteni kanali Mstaafu Issa Machibya, inaonyesha kuwa Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu inaongoza kwa idadi kubwa ya wanafunzi ambao hawajaripoti shule mpaka sasa.

Jumla ya wanafunzi 1,643 sawa na asilimia 52.7% ya wanafunzi 3,107 waliochaguliwa kujiunga kidato cha kwanza mwaka 2014 katika halmashauri ya wilaya ya Kasulu bado hawajaripoti shule.

Hata hivyo karibu halmashauri zote saba za (Kasulu, Buhigwe, Kibondo, Kakonko, Uvinza,Kigoma Vijijini na Manispaa ya Kigoma Ujiji bado idadi ya wanafunzi wasiopripoti ni kubwa.

Halmashauri ambayo inafuatia kwa idadi kubwa ya wanafunzi kutoripoti shule ni Manispaa ya Kigoma Ujiji ambayo wanafunzi 1,539 sawa na asilimia 55.7% ya wanafunzi 2,761 waliochaguliwa bado hawajaripoti, ikifuatiwa na Uvinza ambayo wanafunzi 992 sawa na asilimia 53.3% ya wanafunzi 1,863 waliochaguliwa.

Nyingine ni Halmashauri ya wilaya ya Kigoma Vijijini ambayo wanafunzi 985 sawa na asilimia 67.63% ya wanafunzi 1,459 waliochaguliwa hawajaripoti, wakati halmashauri ya wilaya ya Kibondo wanafunzi 707 sawa na asilimia 44.6% ya wanafunzi 1,572 waliochaguliwa bado hawajaripoti.

Idadi ya wanafunzi ambao hawajaripoti shule kwa wilaya ya Buhigwe ni 603 sawa na asilimia 38.3% ya wanafunzi 1,570 waliochaguliwa, huku wanafunzi 390 sawa na asilimia 46.7% ya wanafunzi 835 waliochaguliwa katika wilaya ya Kakonko wakiwa bado hawajaripoti.

Kati ya wanafunzi ambao hawaripoti shule Wasichana ni 2,592 kati ya 5,054 waliochaguliwa na Wavulana ni 4,267 kati ya 8,113 waliochaguliwa.

Hali hiyo imemlazimu Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Luteni Kanali Mstaafu Issa Salehe Machibya, kukutana na waandishi wa habari na kutoa maagizo mbali mbali ikiwemo kuziagiza halmashauri zote kuhakikisha kuwa wanafunzi wote ambao hawajaripoti wawe wameripoti kabla au ifikapo Februari 15 mwaka huu.

Aidha aliagiza wazazi/Walezi wote ambao watoto wao waliochaguliwa kujiunga kidato cha kwanza na hawajaripoti shule wahakikishe kuwa wanawapeleka shuleni mapema kabla ya tarehe 15, vinginevyo watakamatwa na kufikishwa kwenye vyombo vya sheria.

Aliwataka pia wakuu wa shule watoe ushirikiano kwa wazazi au walezi kuwapokea wanafunzi waliochaguliwa hata kama hawana mahitaji muhimu na kwamba mahitaji hayo yatafuata baadae.

“Nasisitiza kwamba hairuhusiwi kuwafukuza hawa watoto, taratibu za malipo zitafuata tu. Yaani lazima watalipa na huu utaratibu wa kuwatimua timua watoto mashuleni ukome,”alisema Luteni Kanali Mstaafu Issa Machibya.

Aidha aliwataka wazazi kuacha kubweteka na agizo la serikali linalokataza walimu kuwafukuza wanafunzi kwa kukosa ada, bali waweke kipaumbele katika suala la elimu kwa kuwalipia watoto wao ada kwa wakati hasa kwa kuzingatia kuwa elimu ndio ufunguo wa maisha.

Pia amewaagiza wakurugenzi watendaji wote watoe taarifa za awali za utekelezaji wa agizo la Mh.Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na ifike ofisi ya mkuu wa mkoa kabla ya tarehe 15/2/2014, ikionyesha idadi ya wanafunzi waliochaguliwa kwa kila shule, walioripoti, wasioripoti na sababu za kutoripoti zijulikane au kuainishwa kiuhalisia.

By KigomaLive Posted in Elimu

One comment on “Zaidi ya nusu ya wanafunzi hawajaripoti Shule Kigoma

Toa Maoni Yako Kuhusu Habari Hii