Aside

Wafanyakazi kutoka Taasisi mbali mbali umma na binafsi mkoa wa Kigoma, wakiwa wamejumuika pamoja kwenye sherehe za Mei Mosi kwenye viwanja vya Mwanga Community Center.

Wafanyakazi kutoka Taasisi mbali mbali umma na binafsi mkoa wa Kigoma, wakiwa wamejumuika pamoja kwenye sherehe za Mei Mosi kwenye viwanja vya Mwanga Community Center.

 

SHIRIKISHO la Vyama vya Huru vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA), mkoani Kigoma, wameitaka Serikali ipunguze kodi ya mishahara na kuwa chini ya asilimia 10%, kudhibiti mfumo wa bei sambamba na kupandisha mishahara ya wafanyakazi ili kuwapunguzia ukali wa maisha.

Katika risala yao kwenye sherehe za Mei Mosi ambayo ilieleza changamoto zinazowakabili, wafanyakazi wa mkoa wa Kigoma walisema kuwa mishahara ya wafanyakazi ni midogo na kodi ni kubwa ukilinganisha na hali halisi ya maisha ya sasa.

Aidha walieleza kuwa upungufu mkubwa wa wafanyakazi kwenye maeneo mengi ni changamoto kwa wafanyakazi waliopo na baadhi ya viongozi wa kisiasa kuingilia majukumu ya wafanyakazi kinyume na kanuni na sheria.

“Baadhi ya viongozi wa kuchaguliwa wamekuwa wakiwaamuru waajiri hasa wakurugenzi wa halmashauri za wilaya na Manispaa kuwahamisha, kuwasimamisha kazi, kuwafukuza kazi na kuwafungulia mashitaka wafanyakazi bila sababu zozote za msingi,”ilieleza sehemu ya risala hiyo.

Mbali na hayo wafanyakazi mkoni Kigoma pia wameainisha mambo mbali mbali ambayo kama yatatekelezwa changamoto za wafanyakazi ikiwemo gharama kubwa za maisha zitapungua.

Baadhi ya mambo hayo ni kuwataka waajiri wafunge mikataba ya hali bora na vyama vya vya wafanyakazi kwa niaba ya wafanyakazi kwa lengo la kuboresha mishahara na maslahi mengine ya kazi na mikataba hiyo itekelezwe na kuheshimiwa.

Pia wameitaka serikali na waajiri binafsi kuwaendeleza waajiriwa wao kielimu ili waendane na zama hizi za sayansi na teknolojia pamoja na kuondoa vikwazo kwa wafanyakazi wanaopata fursa ya kwenda kujiendeleza na serikali kuwakumbusha mifuko ya hifadhi ya jamii kuwachukulia hatua waajiri wasiopeleka michango ya waajiriwa wao kwenye mifuko husika.

Akiongea kwenye maadhimisho hayo, Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Luteni Kanali Mstaafu Issa Machibya, aliahidi kushirikiana na waajiri na mamlaka zinazohusika kushughulikia masuala yote yaliyoelezwa na wafanyakazi hao.

Kulingana na ripoti ya Global Tax Comparison ya Benki ya Dunia mwaka 2014, wafanyakazi wa Tanzania wanaumizwa sana katika kodi kuliko wafanyakazi wan chi nyingine za Afrika Mashariki.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo wastani wa kodi kwa mfanyakazi wa Tanzania ni asilimia 18%, Uganda asilimia 11%, Kenya asilimia 6.8, Burundi asilimia 10.3 na Rwanda ni asilimia 5.6%.

Wastani wa kodi ya mfanyakazi duniani kwa mujibu wa ripoti hiyo ni asilimia 16.2%. kwa takwimu hizo sio tu kwamba wastani wa kodi ya mfanyakazi wa Tanzania ni kubwa kuliko nyingine Afrika Mashariki, bali ni zaidi ya wastani wa kodi ya mfanyakazi duniani.

Kwa maoni ya wananzuoni kodi ya mshahara wa mfanyakazi inapaswa kushuka kwa asilimia 50%, yaani itoke kuwa asilimia 18% -9% kwa wastani wa kuanzia, lakini kwa mujibu wa taarifa ya Mamlaka ya Mapato nchini (TRA), mwaka jana ni kwamba kama watashusha kodi hiyo kutoka 18%-9%, watapoteza mapato ya kiasi cha shilingi 704 bilioni.

Maoni ya wananzuoni ni kwamba mapato hayo yanaweza kufidiwa kwa kutekeleza sheria ya kodi ya majengo ambayo mpaka sasa utekelezaji wake ni asilimia 3% ambapo shilingi 25 bilioni hukusanywa, na hiyo ina maana kuwa kama sheria hiyo itatekelezwa kwa asilimia 100% zaidi ya shilingi 800 bilioni zitakusanywa.

Tazama matukio mbali mbali ya sherehe za Mei Mosi katika picha:

Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Luteni Kanali Mstaafu, Issa Machibya, akikabidhi zawadi mbali mbali kwa wafanyakazi hodari wakati wa sherehe za Mei Mosi.

Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Luteni Kanali Mstaafu, Issa Machibya, akikabidhi zawadi mbali mbali kwa wafanyakazi hodari wakati wa sherehe za Mei Mosi.

DSC00480

DSC00476

Vijana wa kikosi cha 821 KJ Bulombora, wakitoa burudani ya ngoma kwenye sherehe za Mei Mosi.

Vijana wa kikosi cha 821 KJ Bulombora, wakitoa burudani ya ngoma kwenye sherehe za Mei Mosi.

 

Mishahara midogo, kodi kubwa bado kilio cha Wafanyakazi

By KigomaLive Posted in Habari

Toa Maoni Yako Kuhusu Habari Hii