Mshambuliaji wa Gor Mahia Michael Olunga
ametawazwa kuwa mshindi wa tuzo ya
mwanasoka bora zaidi wa mwaka 2015 nchini
Kenya.
Mshambuliaji huyo wa timu ya Gor Mahia
ametuzwa kombe hilo pamoja na kitita cha
shilingi milioni moja za Kenya au dola elfu kumi
mbali na zawadi nyinginezo kama vile TV kubwa
ya inchi 43.
Sherehe za mwaka huu za kuwatuza wachezaji
bora wa kandanda nchini Kenya zilikuwa za
kipekee kwani mbali na miaka ya nyuma, kitita
kikubwa cha pesa kilitumika kuwapa washindi wa
karibu kila kitengo.
Kulikuwa na jumla ya vitengo 13 vya
kushindaniwa, huku walioibuka washindi
wakipewa pesa taslimu au zawadi chungu nzima
zilizotolewa na kampuni mbalimbali za wafadhili.
Licha ya mwenyekiti wa soka Nchini Kenya Sam
Nyamweya na waziri wa michezo Hassan Wario
wakikwepa kuhudhuria sherehe hizo, zilizofanyika
katika hoteli moja ya kifahari Jijini Nairobi, nyota
wa zamani wa soka nchini Kenya walihudhuria
akiwemo J.J Masiga.
Tuzo ya mwaka huu ya mchezaji bora wa mwaka
lilimwendea chipukizi wa miaka 22 mwanafunzi
wa chuo cha teknolojia cha Kenya na
mshambulizi wa Gor Mahia Michael Olunga.
Tuzo mpya iliyobuniwa mwaka huu ya mchezaji
chipukizi zaidi wa mwaka, ilimuendea George
Mandela wa timu ya Muhoroni FC, kutoka
Magharibi mwa Kenya.
Nayo tuzo ya refa aliyeimarika zaidi mwaka huu,
ilitwaliwa na Raymond Onyango na ile ya naibu
kocha ikatwaliwa na Stephen Deya.
Nayo timu bora zaidi mwaka 2015 ilikuwa
Western Stima baada ya kuzipiku Mathare United
na Sony Sugar.
John Baraza wa timu ya Sofapaka alinyakuwa
tuzo ya mchezaji mwenye nidhamu ya hali ya juu
zaidi mwaka huu.
Ushindani mkali ulishuhudiwa katika tuzo la
maneja bora zaidi wa timu, ambapo hatimaye Bw
Jodali Obondo wa Gor Mahia aliibuka mshindi.
Katika wachezaji, kipa bora mwaka huu wa KPL
alikuwa Bonface Oluoch wa Gor Mahia aliyejipatia
dola elfu tano, huku Farouk Shikalo wa Muhoroni
Youth na Jairus Adira wa wakijipatia dola elfu
mbili kila mmoja.
Mlinzi bora alikuwa mchezaji wa Gor Mahia raia
wa Burundi, Karim Nzigimana.
Tuzo la Kocha bora lilimweendea mkufunzi wa
mabingwa wa ligi kuu nchini Kenya Gor Mahia,
Frank Nutall, ambaye alipewa mkataba huo kwa
misingi kuwa sharti aifanye timu ya Gor kuibuka
mshindi ili apate kazi ya ukufunzi, jambo ambalo
amelitimiza.