Idara ya Uhamiaji kutumia mfumo wa kisasa kutambua raia wa kigeni


Afisa Uhamiaji Mkoa wa Kigoma, Naibu Kamishina wa Uhamiaji, Ebrosy Kingdom Mwanguku, akiongea na Waandishi wa Habari, hawapo pichani.

Afisa Uhamiaji Mkoa wa Kigoma, Naibu Kamishina wa Uhamiaji, Ebrosy Kingdom Mwanguku, akiongea na Waandishi wa Habari, hawapo pichani.

SERIKALI ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Idara ya Uhamiaji itaendesha zoezi la nchi nzima la kuwaandikisha raia wote waishio nchini, kwa lengo la kuiwezesha Serikali ya Tanzania kuboresha uwezo wake katika uendeshaji wa masuala ya uhamiaji.

Akitoa taarifa kwa Vyombo vya Habari Mkoani Kigoma, Afisa Uhamiaji wa Mkoa wa Kigoma, Naibu Kamishina wa Uhamiaji, Ebrosy Kingdom Mwanguku, amesema zoezi hilo litatekelezwa kwa kuratibiwa na Idara ya Uhamiaji na kuendeshwa kwa pamoja na Chuo Kikuu, kituo kinachoshughulikia masuala ya uhamiaji katika shule ya sheria CSFM, na Shirika la Kimataifa la Uhamiaji IOM.

Alisema awamu ya kwanza ya zoezi hilo itahusu mikoa ya Kagera, Kigoma, Tabora na Geita, na kwamba litaanza wakati wowote kuanzia sasa baada taratibu kukamilika.

“Lengo kuu ni kuboresha uwezo wa serikali katika uendeshaji wa masuala ya uhamiaji kwa maana ya uwekaji kumbukumbu, urasimishaji ukaazi na uratibu wa kurejesha makwao wanaohiari au wasiokuwa na sifa za kuendelea kuishi nchini,”alisema Mwanguku.

Alisema zoezi hilo ni la aina yake na linafanyika kwa mara ya kwanza hapa nchini na la kisasa na la kimataifa na kwamba mfumo unaotumika ni mfumo ambao nchi kama China na nyingine za Asia zimeutumia, ambapo mtu akishaingizwa kwenye database, hawezi kufanya udanganyifu.

Aidha alisema miongoni mwa mambo yatakayofanyika katika hatua ya awali ya zoezi hilo ni pamoja na uhamasishaji, kutambua na kuandikisha raia wa kigeni waliomo mijini na vijijini na kuwapatia barua maalum ya utambulisho tayari kwa zoezi la kuandikishwa rasmi ambalo litafanyika ngazi ya kata.

Mengine ni kuwaandikisha na kupata taarifa zao kwa ajili ya kuweko kumbukumbu katika database, kuwasaidia watakaoamua kurejea nchini mwao kwa hiari na kuhakiki ukaazi wa wale wanaotaka kurasimisha au kuthibitisha uhalali wa ukaazi kwa wale wenye hati.

Aidha Naibu Kamishina wa Uhamiaji (Mwanguku), alisema kuwa Idara ya Uhamiaji kwa kushirikiana na serikali za mitaa itaendesha zoezi la awali la uandikishaji kupitia serikali za vijiji/mitaa ambapo wakuu au viongozi wa kaya watatoa idadi na majina ya wategemezi wao, kazi ambayo itafanywa na watendaji wa vijiji.

Nae Meneja Mradi kutoka Chuo Kikuu, kituo kinachoshughulikia masuala ya uhamiaji katika shule ya sheria CSFM,Johnson Brahim, alieleza wajibu wao katika zoezi hilo kuwa ni kufanya uhamasishaji kwa walengwa kuhusu utaratibu mzima wa zoezi, lini uandikishaji utaanza, vituo vitakavyotumika kujiandikisha, muda na maelezo mengine ya jumla kuhusiana na zoezi.

Alisema muda ukifika wote wanaohusika wajitokeze kujiandikisha.
“Muhimu hapa ni kwa wale wanaohusika wajitokeze kwa sababu kwa kujificha maanake ni kwamba iko siku watapata matatizo,”alisema. Brahim.

“Fursa hii imetolewa kama wewe ni mgeni unakwenda kujiandikisha halafu unapata uhalali kiuhamiaji. Kama ni kibali cha ukaazi unapata, kama ni taratibu nyingine pia za kiuhamiaji zinafuatwa. Kwa maana nyingine ukiishi kwa kufuata sheria za nchi hutapata misukosuko wala vyombo vya usalama havitakuwa na tatizo na mtu.”

Kwa upande wake Afisa Miradi wa Shirika la Kimataifa la Uhamiaji IOM, Charles Mkude, ambaye shirika lake linafadhili zoezi hilo, amesema kiasi cha dola za kimarekani milioni moja zinatarajiwa kutumika katika awamu ya kwanza ya zoezi hilo linalohusisha mikoa minne.

“Tumepata fedha kutoka Shirika la Maendeleo la Uingereza, DFID, na nchi nyingine wahisani ambao wametoa fedha ili kuratibu hili zoezi liweze kufanyika katika mikoa minne kwa majaribio na baadaye serikali itapeleka zoezi hili kwenye mikoa mingine,”alisema Mkude.

Alisema Shirika lake pia linatoa ushauri wa kiufundi wa jinsi gani zoezi hilo linaweza kufanyika kwa kuangalia nchi nyingine ambazo zimefanya zoezi kama hilo wamefanikiwa vipi.

Baadhi ya viongozi watendaji na madiwani waliozungumzia zoezi hilo mkoani Kigoma, walisema zoezi hilo lina manufaa makubwa kwa nchi ili kuweza kupata takwimu sahihi za wageni waliopo nchini na kwamba zoezi hilo litafanikiwa kwa sababu linashirikisha viongozi kuanzia ngazi za chini tofauti na zoezi lililopita la operation Kimbunga.

Advertisements
By KigomaLive Posted in Habari

Toa Maoni Yako Kuhusu Habari Hii

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s